WASIFU WA MAREHEMU ALICE WALI KALAGHE MKOBA

Maisha ya Marehemu Mama Alice Wali Kalaghe, ambaye ni mjane wa marehemu Kalaghe Mkoba aliyetokea Kijiji cha Bungule, Kasigau imeambatana sana na historia tata na ya kuhuzunisha, katika maisha ya Wa Kasigau kwa jumla.

Kitambulisho chake cha Uraia wa Kenya, kinathibitisha ya kwamba, alizaliwa mnamo karne moja iliyopita, na miaka kumi na nne juu yake, yaani miaka 114 ambao ni umri mkubwa.

Alikuwa kasichana kadogo, pale wananchi wa Kasigau, kikiwemo kijiji cha Rukanga alikozaliwa, kilipo teswa, na kuadhibiwa vikali na serikali ya Ukoloni, na hatimaye kutoroshwa hadi Malindi kwa madai eti Wakasigau waliwasaliti wanajeshi Waingereza waliokuwa wamepiga kambi milima ya Kasigau, wakipigana vita vikali vya kwanza vya dunia, dhidi ya Wajerumani waliokuwa nchini Tanganyika wakati huo. Ilikuwa kati ya mwaka 1914 hadi 1918.

Marehemu Alice Wali, pamoja na babake aliyejulikana kwa majina Mterengo au, Mtwangi, na mamaye Nose, wakiwemo dada yake Nyasezi na nduguye Ngewe, na wanakijiji wenzao, walikusanywa kwa pamoja na kusafirishwa kwa gari la moshi kotoka Maungu hadi Mombasa, na baadaye kupelekwa kwa meli hadi Malindi walikozuiliwa kwa miaka kadhaa, katika hali duni na ya kuhuzunisha kimwili na kiafya.
Baada ya kupitia majuto hayo kule Malindi, walikoshuhudia maafa kupitia ugonjwa wa Malaria, na kutengwa kijamii, aliandamana na wazazi wake kwenye safari ya kurejea Taita, ilipoamuliwa rasmi waregeshwe makwao. Waliletwa kwanza Mwatate, walikopewa hifadhi, na kazi za ukulima kwenye shamba la mkonge lililoanzishwa na wakoloni.

Baada ya kifo cha wazazi wake, Marehenu Mama Alice Wali alipewa hifadhi, na kusaidiwa na nduguye wa kambo marehemu Mwakulomba, ambaye alimuoza kwa marehemu Kalaghe Mkoba kama muke wa pili, kwenye miaka ya 1920s.

Mama Alice Wali a mumewe Kalaghe Mkoba walibarikiwa na watoto tisa (9), ambao watatu wao-Maghanga, Peter Makalo, na Robert Mwavula, walizaliwa Mwatate, kabla ya jamii yake kurudi kwao kijiji cha Bungule, Kasigau. Watoto wake waliozaliwa Bungule ni: marehemu Jones Kea, Grace Akora (mke wa Mwaighuri), marehemu Mwanjala, marehemu Nose (mke wa Lotoi) aliyeolewa Turkana, Cosmas Mdari (Polisi mstaafu) na kitinda mimba Rehema Mwachidzo (Damaris Mwakuli). Bwana yake, Mzee Kalaghe Mkoba, alifariki dunia mwaka 1963, hivyo kumwacha Mama Alice Wali akiendelea na maisha yake ya ukulima nay a kulea watoto wake hodari katika masomo.

Aliposogelea na kufikisha umri wa miaka mia moja (100) , alikuwa tayari ameshawacha ukulima, na badala yake, alifurahia ulezi wa wajukuu, vitukuu, na vilembwe wake. Alijiingiza pia kwa maswala ya dini, akiwa mshiriki wa dhehebu la kanisa la Ebenezer linaloongozwa na Mchungaji Chrispus Mwakisambi.

Mama Alice Wali alionekana mcheshi, na mwenye nguvu, na afya tele tele. Mwanawe Cosmas Mdari, kwa mfano, aliyejenga Bamburi, kitongoji cha Mombasa, baada ya kustaafu mwaka 2005, anakumbuka maombi yake ya nguvu kabla ya chakula, alipowatembelea nyumbani kwake huko Bamburi. Enzi hizo aliendelea kujilisha mwenyewe, na aliendelea kuwasiliana nao bila ya kigugumizi, au, ulemavu wowote.

Lakini, baada ya kifo cha mjukuu wake mwalimu Ben Kalaghe mnamo mwaka wa 2007, Mama Alice Kalaghe alionekana kujawa na huzuni nyingi mno, ambayo haikuisha akilini mwake. Aliendeelea kumuomboleza kwa muda mrefu, kiasi cha kuchangia pakubwa hali yake ya kiafya iliyozidi kuzorota.

Takriban miaka kumi iliyopita, Mama Alice Wali, ambaye alishapoteza mach yake na kutosikia kutokana na uzee na hali yake duni ya afya, alifurahia sana kuishi karibu na mwanawe Grace Akora (mke wa Mwaighuri) anayefahamika Zaidi kama “ Mee Julius”, aliyeolewa Makwasinyi. Alivyozidi kuzeeka, ndivyo roho yake ilivyopenda pia kujichagulia vyakula. Lakini mara kwa mara, alikataa kata kata, kula chakula chochote.

Kufikia Jumapili, mnamo tarehe 28 Oktoba, 2018, kwenye masaa ya sa kumi na moja alfajiri (5.00 am), Mama Alice Wali Kalaghe aliaga dunia.

Amewacha watoto watatu, yaani Grace Akora Mwaighuri (Mee Julius), Cosmas Mdari, na Rehema Mwachidzo (Damaris Mwakuli), pamoja na wajukuu 73, vitukuu 250, na vilembwe 59.

Mwenyezi Mungu aipumzishe Roho yake vyema Peponi!